Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa Ethiopia azindua kiwanda kikubwa zaidi cha saruji nchini humo kilichojengwa na Kampuni ya China
ADDIS ABABA – Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezindua Kiwanda cha Saruji cha Lemi kilichojengwa na Kampuni ya China, ambacho ni kikubwa zaidi cha aina yake nchini humo chenye uwezo wa kuzalisha saruji ya tani 15,000 kwa siku.
Akizindua kiwanda hicho Jumamosi, Abiy amesema "mradi huo unatoa mfano wa ukamilishaji wa haraka na wenye ufanisi wa miundombinu muhimu. Hongera kwa wote waliohusika katika kufanikisha mradi huu muhimu, ambao sasa unazalisha asilimia 50 ya saruji yote inayozalishwa kote nchini."
"Ninaporudi kwenye eneo hili la mradi baada ya miaka miwili, nimestaajabishwa na hatua iliyopigwa, ambayo inaakisi kanuni zetu za utawala. Inaonyesha kwamba kwa kufanya kazi kwa bidii, vizazi vijavyo havitarithi umaskini bali msingi wa ukuaji na ustawi," amesema Waziri Mkuu huyo katika hotuba yake.
Kikiwa kinamilikiwa kwa ubia wa Kampuni Hodhi ya West International, ambayo ni kampuni tanzu barani Afrika ya Kampuni ya Saruji ya West China, na Kampuni Hodhi ya Afrika Mashariki, Kiwanda cha Saruji cha Lemi kiliripotiwa awali kugharimu dola milioni 600 za Kimarekani. Kiwanda hicho kiko katika Eneo Maalum la Viwanda vya Vifaa vya Ujenzi la Lemi, umbali wa kilomita takriban 150 kaskazini mwa mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Ahmed amesema kuja kwa miradi ya kiviwanda kama vile Kiwanda cha Saruji cha Lemi nchini humo, kutatoa mchango usio wa mfano katika kutoa nafasi za ajira na maendeleo ya taifa, hasa katika sekta kama vile utengenezaji wa chuma na uzalishaji wa mbolea, ambayo inaweza kuchochea mapinduzi makubwa ya viwanda na kilimo.
Akibainisha kuwa changamoto zinazokabili nchi kama Ethiopia zinahitaji masuluhisho makubwa, Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia amesema ushirikiano wa pamoja kati ya sekta binafsi na ya umma ni muhimu katika kufungua fursa za nchi na kushughulikia matatizo yanayokabili nchi hiyo.
"Kwa kuwekeza katika mipango kama hii, tunaweza kunufaisha watu wengi zaidi na kuhakikisha wanaishi maisha yenye heshima," Abiy amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma